WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia sheria na miongozo ya vyombo vya habari, ikiwemo kuepuka maudhui ya chuki, ubaguzi, kashfa, matusi na uchochezi wa vurugu wakati wa kuripoti Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Wito huo umetolewa Agosti 11,2025 na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Egbert Mkoko, wakati wa kikao kazi cha mafunzo kwa mabloga kuhusu uandishi wa habari katika kipindi cha kuelekea uchaguzi.
Dkt. Mkoko amesema mwongozo huo, uliotayarishwa na Idara ya Habari (MAELEZO) kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC), unalenga kuimarisha weledi na maadili ya uandishi ili kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki na amani na utulivu.
“Epukeni kueneza uvumi usio na uthibitisho, epukeni kubashiri matokeo, na hakikisheni mnasoma sheria za uchaguzi,” amesema Dkt. Mkoko
Amefafanua kuwa mwongozo huo unasisitiza kuchapisha taarifa za kweli, sahihi na zilizothibitishwa kikamilifu, pamoja na kuepuka upendeleo na habari zinazoweza kuathiri mshikamano wa kijamii.
Lengo kuu, amesema, ni kuweka misingi ya kitaaluma, kimaadili, usawa, uwazi na weledi katika kuripoti uchaguzi, sambamba na kulinda haki ya wananchi kupata habari sahihi na zenye kuaminika
