Na MWANDISHI WETU
Huku tarehe ya kupiga kura ikikaribia, Tume Huru ya
Uchaguzi (INEC) imethibitisha kuwa hamasa ya wananchi kushiriki katika kutimiza
wajibu wao wa Kikatiba ni kubwa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 5(1),
inampa kila raia mwenye umri wa miaka 18 na zaidi haki ya msingi ya kupiga
kura. Aidha Kauli za wananchi waliohojiwa zimeonyesha utambuzi wa kina wa
umuhimu wa haki hii.
Mkazi wa Goba mkoani Dar es salaam,John James amesisitiza
umuhimu wa kila mtu kushiriki: “Kupiga kura ni haki ya msingi. Ukikosa kupiga
kura, unampa mwingine ruhusa ya kukuamulia kiongozi. Ni wajibu wetu kila mmoja
kwenda kupiga kura kwa maendeleo ya nchi yetu.”
Khadija Suleiman, Mama Lishe kutoka Gongolamboto,
anaelezea matarajio yake ya mabadiliko kupitia sanduku la kura: "Nitapiga
kura Oktoba 29 kuchagua viongozi wanaojua shida za wananchi kama sisi. Tunataka
viongozi wanaojali barabara, maji na mikopo kwa wanawake."
Kauli hizi zinadhibitisha kuwa Watanzania wanaona kura
kama njia halali na ya amani ya kudai mabadiliko na maendeleo, na si kupitia
maandamano, vurugu, wala jazba.
Tanzania: Nguzo ya Amani Afrika
Tanzania imejijengea heshima kubwa kimataifa kama mfano
wa demokrasia barani Afrika, hasa kwa uwezo wake wa kuendesha chaguzi kwa
amani, utulivu na utawala wa sheria.
Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa dhamira hii ya
Watanzania kutimiza wajibu wao kwa amani inathibitisha kuwa: "Watanzania
hawatapigana; watapiga kura."
Kwa kuwa kura ni silaha muhimu ya kidemokrasia, Serikali
na wadau wa demokrasia wamewataka Watanzania wote—vijana, wazee,
wafanyabiashara, na wakulima kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, kupiga kura kwa
utulivu, na kisha kurudi majumbani kwa heshima ya taifa.
Kura yako ni sauti yako. Sauti yako ni nguvu ya taifa.
Usiiache.
