SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mabadiliko makubwa ndani ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidao, imeeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, amejiuzulu wadhifa wake kufuatia mvutano wa muda mrefu kuhusu upangaji wa mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga na Simba.
Wakati Kidao akitangaza kupokea barua ya kujiuzulu wadhifa wake Steven Mguto, Rais wa TFF, Wallace Karia, amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo.
Awali Yanga walieleza kutoridhishwa na uamuzi wa TPLB, ikiwemo kuhamishwa kwa tarehe ya awali ya mechi hiyo ambayo ilikuwa Machi 8, lakini baadaye ikaahirishwa bila maelezo ya kina yanayoeleweka kwa pande zote.
Baada ya sintofahamu hiyo kuendelea kushika kasi na klabu ya Yanga kuonyesha kutokuwa na imani na viongozi hao, hatimaye mchezo huo ulipangwa tena kufanyika kesho, Jumapili, Juni 15, kabla ya kusogeza mbele tena hadi Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

